Pakua sasa Bandarini SACCOS App  ufurahie huduma zetu kupitia simu yako ya kiganjani

BANDARINI SACCOS LTD YAKABIDHI ZAWADI KWA MLEZI WA CHAMA CHA USHIRIKA CHA BANDARINI SACCOS

BANDARINI SACCOS LTD YAKABIDHI ZAWADI KWA MLEZI WA CHAMA CHA USHIRIKA CHA BANDARINI SACCOS

Tarehe 10.01.2024 Uongozi wa Bandarini SACCOS Ltd ulikabidhi zawadi ya ngao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliyotolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa 55 uliofanyika tarehe 26 Novemba 2023 katika Ukumbi wa Bandari Tower Jijini Dar es Salaam.

Zawadi hii ilitolewa mahsusi kutambua na kuenzi mchango wa Mkurugenzi Mkuu ambaye ni Mlezi wa Bandarini SACCOS. Ambapo Mlezi wa chama amekuwa chachu na  ametoa mchango mkubwa sana kwa chama pamoja na wanachama katika kukiwezesha chama kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama na pia kustawisha maslahi ya watumishi ambayo yamewawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama.

Katika salamu za Mwenyekiti wa Bandarini SACCOS za kukabidhi zawadi hiyo alipata wasaa wa kumpongeza Mlezi wa chama kwa kusema “Wewe umekuwa na mtazamo chanya kwa chama jambo lililopelekea sisi kutimiza wajibu wetu kwa urahisi na kuwezesha chama kutimiza majukumu yake kwa wanachama”.

Aidha, aliendelea kueleza kuhusu mipango ya chama iliyopo kwa sasa ambayo anatambua ni muendelezo wa jitihada za pamoja ambazo ni kuendelea kuboresha mifumo hususan ya TEHAMA ili kuongeza kasi ya kutoa huduma, kuongeza ubunifu wa bidhaa na huduma ili kuwezesha wanachama kupata wigo mpana wa huduma, kuendelea kuongeza wigo wa mapato ili kupunguza gharama za huduma ikiwa ni pamoja na kupunguza riba, na kuendelea kuimarisha utawala bora na uwazi ili kuimarisha afya ya rasilimali za chama na wanachama.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa chama alitoa salaam na pongezi zake kwa mlezi wa chama kwa niaba ya viongozi wengine, wanachama na wafanyakazi wa Bandarini SACCOS akieleza walivyo na imani kubwa kwake katika kustawisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandarini Tanzania ili kufanikisha uendelevu wa Bandarini SACCOS. Makamu Mwenyekiti katika salam hizo alisisitiza kwa kusema “Sisi viongozi, wanachama na wafanyakazi kwa ujumla tunakuombea afya na ustahimilivu wa kuendelea kuwatumikia Watanzania ambao miongoni mwao ni wanachama wetu wa Bandarini SACCOS”.

Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ambaye ni Mlezi wa Bandarini SACCOS alipata wasaa wa kushukuru kwa kutambua mchango wake katika kusimamia na kuimarisha utendaji kazi wa Bandarini SACCOS. Katika maneno yake ya shukrani alisema “Nawashukuru kwa kutambua umuhimu wa haya tunayofanya kwa ajili ya Bandarini SACCOS nawaahidi kuendelea na ushirikiano huu ili niendelee kuiona Bandarini SACCOS ikishamiri na ikiwezekana ifikie hatua ya kuwa Benki ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania”

Post a Comment

Translate »