Uanachama wa Bandarini SACCOS Limited upo wazi kwa mtu yeyote anayekidhi vigezo vilivyowekwa katika ibara ya 10 ya Masharti yake, mwenye sifa stahiki, na aliye tayari kuzingatia masharti hayo na kunufaika na huduma zinazotolewa.
Bandarini SACCOS Limited inaendeshwa na wanachama wake, ambao kupitia Bodi ya Uongozi wameweka Sera, Miongozo, na Maamuzi mbalimbali ya kusimamia chama. Utekelezaji wa mambo haya unafanyika kupitia vikao na mikutano kwa mujibu wa Kanuni na Masharti yaliyopo. Uongozi unazingatia ushirikishwaji wa wanachama wote na kuheshimu maamuzi ya wengi, bila kuzingatia hali ya kifedha ya mwanachama au cheo chake ndani ya chama.
Chama kitasisitiza ushirikiano wa wanachama katika kujenga Mtaji wake wa Msingi kwa usawa, kulingana na hisa wanazomiliki, ili kumiliki mali za chama kwa pamoja. Pia, kitaendelea kuhamasisha wanachama kushiriki katika shughuli za kiuchumi ili kuchangia uzalishaji wa ziada ya chama na kugawana faida hiyo kwa mujibu wa Sheria, miongozo ya kiushirika, na masharti husika.
Sehemu ya Mtaji wa chama itakuwa ya umiliki wa pamoja kwa wanachama wote, ikiwa ni Mtaji wa Kitaasisi unaotokana na mgawanyo wa kisheria wa ziada ya mapato kila mwaka, ruzuku za serikali, au misaada kutoka kwa wahisani. Hata hivyo, Mtaji wa Msingi utaendelea kumilikiwa binafsi na kila mwanachama kulingana na idadi ya hisa zake, kama itakavyoainishwa katika Hati yake ya utambuzi.
Bandarini SACCOS Limited ni taasisi huru ya kifedha inayojitegemea, ikifuata falsafa ya ushirika ya kujisaidia (People helping people) katika utoaji wa huduma zake. Iwapo kutakuwa na haja ya kushirikiana na Serikali, taasisi nyingine, au watu binafsi kwa ajili ya kuwezeshwa, itaweza kufanya hivyo. Hata hivyo, maamuzi ya mwisho yatabaki mikononi mwa wanachama bila kuathiri uhuru wao wala misingi ya kidemokrasia katika kujitawala.
Bandarini SACCOS Limited daima itaweka kipaumbele na kuzingatia kwa umakini suala la elimu ya ushirika kwa kuingiza katika shughuli zake za kila siku programu za mafunzo na elimu ya ushirika. Pia, itahakikisha inatoa taarifa kuhusu shughuli zake kwa makundi ya kijamii na kiuchumi ndani ya maeneo yake ya kazi. Lengo la elimu ya ushirika ni kuhamasisha maendeleo kwa wanajamii, wakiwemo wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na maeneo mengine yanayozunguka ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania. Hatua hii inalenga kuongeza uelewa wa fursa zilizopo ndani ya Chama na hatimaye kuvutia wanachama wapya kujiunga.
Kwa kuzingatia msingi huu wa kimataifa, Bandarini SACCOS Limited itaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wajasiriamali kujiunga na Chama na kushiriki katika mitandao mingine ya ushirika yenye faida. Aidha, Chama kitaendeleza uhusiano wa karibu na taasisi zingine za ushirika, ndani na nje ya sekta, katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, kwa lengo la kuimarisha na kukuza ushirika nchini.
Chama hiki ni Ushirika ulioanzishwa na wanachama wake, wengi wao wakiwa wakazi wa Halmashauri zote za wilaya katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mikoa mingine inayopakana na maziwa makuu, sambamba na wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania. Wanachama wake kwa ujumla ni waajiriwa, huku baadhi yao wakijihusisha na shughuli ndogo ndogo za kilimo, usindikaji, ufugaji, na biashara.
Sera na mikakati ya uendeshaji wa Chama huamuliwa na wanachama kupitia vikao vya uongozi na mikutano mikuu ya wanachama na wawakilishi wao. Sehemu ya mafanikio ya kiuchumi ya Chama hutumika kusaidia jamii kwa kuwekeza katika sekta za elimu, afya, mazingira, na shughuli za kiuchumi ili kupanua fursa za maendeleo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza pengo la umasikini miongoni mwa jamii za Kitanzania